WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amekuwa miongoni mwa mamia ya waombolezaji walioshiriki maziko ya mbunge wa zamani, Beatrice Shelukindo (58) yaliyofanyika nyumbani kwa wazazi wake katika kata ya Olorien Jijini Arusha jana.
Viongozi wengine waliohudhuria maziko hayo yaliyotanguliwa na ibada ni pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Jaji Mkuu mstaafu, Agustino Ramadhani, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda.
Pia maziko hayo yalihudhuriwa na wabunge na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka Mkoa wa Tanga na Arusha, Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Kalisti Lazaro na viongozi wengine wa vyama vya siasa na serikali.
Ibada ilifanyika katika Kanisa Kuu la Anglikana, Dayosisi ya Mount Kilimanjaro ambako Askofu mstaafu, Simon Makundi, alisema Beatrice hakuwa fisadi na alitoa mchango mkubwa kwa familia, dini, taifa na Afrika Mashariki.
“Jiulize wewe una mchango gani hata katika familia yako, dini yako, taifa hili na hata kwa Afrika Mashariki?” Alihoji Makundi.
Aliwataka mamia ya waombolezaji wakipewa nafasi, heshima na vyeo serikalini au katika kampuni yo yote kuitunza heshima hiyo kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kuwa na hofu ya Mungu.
Beatrice aliyezaliwa mwaka 1958 amefariki akiwa na umri wa miaka 58, jambo ambalo askofu mstaafu alisema hiyo ni neema ya Mungu.
Alisisitiza kuwa Beatrice alifanya kazi za utumishi serikalini na ubunge kwa uadilifu mkubwa na kupata heshima na serikali, dini na jamii na ndiyo maana aliweza kuhitimisha heshima hiyo hadi mwisho. Askofu Makundi alisema alipata bahati ya kuzungumza naye kabla ya mauti.
UNGANA NASI FACEBOOK KWA KULIKE PAGE YETU
Chapisha Maoni