Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA ), kimefungua kesi ya madai mahakama kuu kanda ya Mwanza ya kupinga amri ya jeshi la Polisi nchini kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa, iliyotolewa juni 7 mwaka huu na kamishna wa polisi Operesheni na Mafunzo Nsato Mssanzya.
Kesi hiyo ya madai namba 79 ya mwaka huu, imefunguliwa leo majira ya saa tisa alasiri na mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA Mh. Freeman Mbowe kwa niaba ya chama hicho, ikiwa ni siku chache baada ya jeshi la polisi wilayani Kahama mkoani Shinyanga kusambaratisha kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwasha wananchi waliokuwa wamejiandaa kuhudhuria mkutano wa uzinduzi wa operesheni okoa demokrasia katika uwanja wa CDT mjini Kahama.
Viongozi wakuu wa chama hicho walioongozana na mwenyekiti wa Taifa CHADEMA kwenda mahakamani kufungua kesi hiyo ni pamoja na makamu mwenyekiti wa chama hicho upande wa Zanzibar Said Issa Mohamed, Katibu mkuu wa CHADEMA Dk. Vicent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, mwenyekiti wa BAVICHA Patrobas Katambi, mwenyekiti wa BAWACHA Mh. Halima Mdee na baadhi ya wabunge wa chama hicho.
Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Mh. Freeman Mbowe amesema kesi hiyo itasimamiwa na mawakili watatu ambao ni Gaspar Mwanalyela, John Mallya na Paul Kipeja.
Mh. Mbowe pia ametumia fursa hiyo kumjibu naibu spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Akson Tulia, kuhusiana na suala la posho za wabunge hasa wa kambi ya upinzania wanaosaini mahudhurio na kisha kutoka nje ya ukumbi wa bunge.
UNGANA NASI FACEBOOK KWA KULIKE PAGE YETU
Chapisha Maoni