Featured
Loading...

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Alhamisi ya July 21




Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Yagoma Kuzungumzia Hatima ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dk Ramadhani Dau

Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) imesema kuwa haiwezi kuzungumzia lolote kuhusu hatma ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dk Ramadhani Dau kwa vile si mwajiriwa wao. 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana kwa simu, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Samwel Wangwe alisema bodi inashughulika na wafanyakazi wa sasa katika shirika hilo na siyo walioondoka. 

“Bodi haiwezi kuchukua hatua dhidi yake (Dk Dau).Vyombo husika ndivyo vitaamua kuhusu hilo,” alisema Profesa Wangwe alipoulizwa kuhusu hatma ya Dk Dau ambaye alikuwa bosi na msimamizi mkuu wa menejimenti iliyosimamishwa kazi. 

Pia, katika kipindi ambacho Dk Dau alikuwa mkurugenzi mkuu, aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi iliyopaswa kutoa idhini ya ujenzi wa kila mradi uliopangwa alikuwa Abubakar Rajabu. 

Profesa Wangwe alisema hayo alipoulizwa kuhusu hatma ya Dk Dau baada ya bodi hiyo juzi kuwasimamisha wakurugenzi sita wa shirika hilo na mameneja sita kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi. 

Dk Dau amekuwa mkurugenzi mkuu wa NSSF kwa miaka kadhaa hadi Februari mwaka huu alipoondolewa baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa balozi, ingawa bado hajapangiwa nchi. 

Katika kipindi alichoondolewa NSSF, ripoti ya ukaguzi uliofanywa na kampuni ya Ernst & Young kwa hisani ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilivuja ikionyesha ubadhirifu wa fedha katika miradi mikubwa ya ujenzi wa majengo ya kisasa yakiwemo ya mji mpya wa Kigamboni jijini Dar es Salaam uitwao Dege Eco Village.

Miradi mingine ambayo ilichunguzwa na CAG akatilia shaka ni ujenzi mradi wa Arumeru, Arusha ambapo NSSF ilikubali kujenga majengo ya kisasa katika viwanja vya mbia mwenzake kampuni ya Azimio Housing Estate Limited ambavyo ekari moja ilithaminishwa kwa Sh1.8 bilioni.

Hata hivyo, mradi huo wenye thamani ya Sh7.2 trilioni ulisimamishwa Januri mwaka huu. 

Machi 19, Rais John Magufuli alimteua Profesa Godius Kahyarara kuchukua nafasi ya Dk Dau na Juni 28, Profesa Wangwe aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi. Uteuzi wake ulianza Mei 30. 

Bodi ya NSSF, katika kikao cha 106 kilichoketi Julai 15, chini ya Profesa Wangwe ilijadili ripoti mbalimbali na kufikia hatua ya kuwasimamisha vigogo hao ikisema mbali ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi pia wanakabiliwa na tuhuma za kutofuata kanuni, sheria na taratibu za manunuzi katika uwekezaji na usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na ajira. 

Wakurugenzi waliosimamishwa ni Yacoub Kidula (Mipango, Uwekezaji na Miradi), Ludovick Mrosso (Fedha), Chiku Matessa (Rasimali Watu na Utawala), Sadi Shemliwa (Udhibiti Hadhara na Majanga), Paulin Mtunda (Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani) na Crescentius Magori (Uendeshaji).

 Mameneja waliosimamishwa ni Amina Abdallah (Utawala), Abdallah Mseli (Uwekezaji), John Msemo (Miradi), Davis Kalanje (Mhasibu Mkuu), Chedrick Komba (Meneja Kiongozi Temeke) na Mhandisi John Ndazi ambaye ni meneja mradi.

Taarifa zaidi zilizopatikana zilieleza kuwa baadhi ya maofisa wa shirika hilo walifikishwa juzi katika Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma ambazo hadi jana hazikuwa zimewekwa wazi. 

Mkurugenzi wa Mawasiliano Takukuru Mussa Misalaba alipoulizwa alisema hawezi kusema ndiyo au hapana, lakini hiyo ipo chini ya taasisi hiyo. 

“Siwezi kukutajia majina kwamba nani na nani wanachunguzwa na Takukuru, sababu kufanya hivyo ni kuwadhalilisha. Kwa kifupi hiyo ni kazi yetu,” alisema. 

Aidha, Profesa Wangwe alisema maofisa hao waliosimamishwa kazi juzi kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi, watachunguzwa na vyombo kulingana na aina ya makosa yao. 

Alipoulizwa kuhusu vyombo vinavyowachunguza maofisa hao alisema hafahamu ni vipi na ni vingapi. 

“Vyombo vinavyohusika vitafanya uchunguzi kulingana na aina ya tuhuma zinazowakabili. Siwezi kusema ni vingapi,”alisema Profesa Wangwe. 

Kwa mujibu wa ripoti kamili ya CAG, Profesa Mussa Assad iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma Aprili mwaka huu, kuna utata wa ardhi ya mradi mpya wa mji wa Kigamboni unaojengwa na NSSF kwa ubia na kampuni ya Azimio Housing Estate. 

Ramani ya mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani 653.44 milioni (Sh1.254 trilioni) inaonyesha utakapokamilika utachangia kubadili sura ya jiji la Dar es Salaam kwani kutakuwa na nyumba za kifahari, majengo ya hoteli, maduka makubwa, eneo la wazi la mapumziko, baa, shule, hospitali, kumbi za mikutano, nyumba za ibada na migahawa. 

Profesa Assad katika ripoti hiyo alitilia shaka uhalali wa Azimio kumiliki ekari 20,000 za ardhi ambazo imetoa kama sehemu ya asilimia 20 ya mchango wake katika mradi huo na kwa kuanzia imetoa ekari 300. 

“Ukaguzi wa hatimiliki umeonyesha kuwa Azimio inamiliki viwanja viwili, kiwanja chenye hatimiliki Na. 81828 chenye ukubwa wa hekta 1.98 na chenye hatimiliki Na. 105091 chenye ukubwa wa hekta 114.11,” anasema CAG. 

“Viwanja vyote vinapatikana katika eneo la Rasi Dege ambavyo kwa pamoja vilihamishiwa kwa Hifadhi Builders kutoka kwa Azimio kwa ajili ya Awamu ya Kwanza ya mradi. 

"Kwa kutumia kizio cha ekari 2.47 kwa hekta, hatimiliki hizi zitakuwa na ukubwa wa jumla wa ekari 286.74, pungufu ya ekari 13.26 kutoka kwenye ekari 300 ambazo zilipangwa kwa ajili ya awamu ya kwanza ya mradi,” anafafanua CAG. 

CAG anasema katika kipindi chote cha ukaguzi wa mradi huo ulioanzishwa mwaka 2014, hakuwahi kupatiwa hatimiliki za ardhi ambayo Azimio aliahidi kutoa kama uchangiaji wa mtaji. 

Vilevile, CAG aliitaka NSSF kuhakikisha inakirejesha katika muda uliopangwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 20.1 (Sh43.9 bilioni) ambazo iliilipa Azimio kwa ushauri wa ujenzi wa mradi wa mji wa Arumeru, Arusha.

“Katika ukaguzi imeonekana Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii limepokea upembuzi yakinifu wa mradi pendekezwa kutoka Azimio Housing Estate Ltd kupitia barua yake ya Mei 16, 2013 yenye kumbukumbu Na. Azimio/NSSF/Arumeru/13/5. Bodi ya Wadhamini iliidhinisha kuingiza katika ubia ardhi iliyotolewa na kampuni ya Azimio katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Mwanza na Arusha kwa ajili ya uwekezaji unaofanana na huu,” anasema. 

“Ada ya ushauri kwa ajili ya kubuni mradi huo ni Dola za Marekani milioni 218.09 (Sh 468.9 bilioni) na ilipangwa Sh 2.4 bilioni zitumike katika awamu ya upangaji wa mradi. Hata hivyo, kiasi hicho kiliongezwa hadi kufikia Sh 102 bilioni bila ya idhini ya Bodi,” anaeleza.
 
Kwa kuwa baadaye NSSF na Azimio walikubaliana kufuta mradi wa Arumeru wenye thamani ya Sh 7.2 trilioni huku Sh43.9 bilioni zikiwa zimetolewa, CAG ameitaka NSSF kuhakikisha mbia huyo anazirejesha katika muda wa miaka mitatu kwa kuangalia riba iliyoko katika soko la wakati huo. 

Orodha ya wanachuo wanaorudi kusoma stashahada maalum ya ualimu UDOM

==> Kuona Majina ya Waliohamishiwa Vyuo vingine  << BOFYA  HAPA>>

==> Kuona majina ya ambao hawajakidhi vigezo vya kurudishwa  << BOFYA HAPA>> 

Majina ya wanachuo waliokuwa wanasoma stashahada maalum ya ualimu chuo kikuu cha Dodoma waliopangiwa kurudi kwenye chuo hicho.  Ibonyeze Picha Kifanya iwe Kubwa zaidi  ili usome vizuri


==> Kuona Majina ya Waliohamishiwa Vyuo vingine  << BOFYA  HAPA>>

==> Kuona majina ya ambao hawajakidhi vigezo vya kurudishwa  << BOFYA HAPA>>

Serikali Kununua RADA Mbili Mpya

SERIKALI imetangaza kununua rada mbili mpya kwa ajili ya kusaidia kukusanya mapato, zaidi ya Sh bilioni 18 ambazo zinapotea kila mwaka kutokana na kukosekana udhibiti katika anga la Tanzania.

Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Ujenzi na Teknolojia, Edwin Ngonyani,  kwenye mkutano uliowakutanisha wataalamu wa masuala ya anga pamoja na wamiliki wa kampuni za ndege barani Afrika.

Alisema katika awamu ya kwanza, Serikali imetenga bajeti kwa ajili ya kununua rada mbili ambazo zitafungwa kwenye viwanja vya ndege vya Mwalimu Julius Nyerere na Kilimanjaro (KIA), huku awamu ya pili ikifungwa katika viwanja vya Mwanza na Songwe.

“Serikali tayari imeshatenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha kuwa inanunua rada mbili, ili kuokoa kiasi cha takribani bilioni 18/- ambazo zimekuwa zikipotea kila mwaka, jambo ambalo linafanya nchi kupoteza mapato, kwani inakuwa haiwezi kulisimamia anga lake lote na hivyo kufanya ndege, hata zile zisizotua nchini huku zikitumia anga hilo, kushindwa kulipa ushuru.

“Kwa sasa Kenya na Rwanda ndiyo nchi zenye rada hizo licha ya kuwa nchi hizo ni ndogo ukilinganisha na Tanzania, rada hizi kila moja inauzwa dola za Marekani milioni 24. Unapoagiza unatakiwa kulipia nusu ya gharama na pindi inapokamilika unamalizia nusu iliyobaki,”alisema Naibu Waziri Ngonyani.

Kwa upande wake, Mkurungezi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TCAA), Hamza Johari, alisema kuwa ununuzi wa rada hizo utasaidia kuongeza mapato na hivyo kufanya viwanja vya ndege kujiendesha vyenyewe bila kusubiri msaada kutoka serikalini.

Katika hatua nyingine, Johari alisema kuwa mamlaka hiyo imesema Tanzania bado haijafikia kiwango cha utengenezaji ndege na hivyo kuwapiga marufuku wanaofikiria kuzitengeneza bila kuwa na kibali cha mamlaka hiyo.

“Ili kuunda ndege unatakiwa kuwa na zana za kisasa… Kwa Tanzania bado hatujafikia uwezo huo, hivyo kama TCAA tunatoa wito kwa wale wote wanaotaka kufanya hivyo bila kushirikisha mamlaka, kuacha mara koja mpango huo kwani ndege hizo wanazotengeneza bila kufuata taratibu, ni hatari na zinaweza zisimudu kukaa hewani muda mrefu na hivyo kusababisha hatari kubwa.

“Hivyo kama mtu anafikiri kuwa ana mawazo ya kutaka kutengeneza ndege, ni lazima aanzie kwetu ili tumshauri kupitia wataalamu wetu na si vinginevyo,” alisema Johari.

Mkutano huo ulikuwa ukikutanisha wamiliki wa ndege zilizokidhi vigezo na wadau mbalimbali wa masuala ya anga kutoka kote Afrika, ukiwa na lengo la kujadili changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo.

Mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma Yaongoza Kwa Mapenzi ya Jinsia Moja


Takwimu zilizotolewa na wizara ya afya, maendeleo ya jamii jinsia , watoto na wazee nchini zinaonyesha kuwa mkoa wa Dar es salaam na Dodoma inaongoza kwa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam waziri wa wizara hiyo Mhe. Ummy Mwalimu alisema kutokana na hali hiyo wizara imepiga marufuku matumizi ya vilainishi vinavyotumiwa na baadhi ya makundi yanayo jihusisha na vitendo hivyo.

Mhe. Ummy Mwalimu alisisitiza kuwa serikali imeamua kuzuia vilainishi hivyo kwani vimetajwa kuchochea vitendo hivyo ambavyo nikinyume na sheria na taratibu za nchi nakuongeza kuwa vitendo hivyo nimiongoni mwa sababu inayochangia ongezeko la VVU.

Aidha Mhe. Ummy alisema kuwa kwa sasa serikali inajikita kuhakikisha kuwa inajenga wodi za wazai, kununua vifaa tiba, madawa ya kutosha katika hosptali zake na sio ununuzi wa vilainishi hivyo.

Mahakama Yatoa Hati ya Kukamatwa Meneja wa Diamond ‘Babu Tale’


MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa hati ya kukamatwa kwa Hamis Tale ‘Babu Tale,’ ambaye ni meneja wa mwanamuziki wa bongo fleva,Diamond Platnumz.

Mahakama imetoa hati hiyo kutokana na Babu Tale kutotii amri ya mahakama iliyomtaka amlipe Shekhe Hamis Mbonde Sh. 250 milioni.

Babu Tale anatakiwa alipe fedha hizo kutokana na kuvunja mkataba kati yake na Shekhe Mbonde, kwa kuuza na kusambaza nakala za mawaidha (DVDs) bila ridhaa ya shekhe huyo, jambo ambalo ni kinyume na haki miliki.

Kutokana na Babu Tale na mwenzake Iddi Tale kushindwa kulipa fedha hizo kama ilivyoamriwa tarehe 18, Februari  mwaka huu, mahakama ilitoa hati ya kukamatwa kwa wadaiwa hao tarehe 8 Julai mwaka huu.

Katika hati hiyo, mahakama ilimuelekeza Kamanda wa Polisi Kanda ya Ilala kuwa, hadi jana tarehe 19 Julai mwaka huu awe amewakamata wadaiwa hao ili wafike mahakamani kueleza kwanini wasipewe adhabu kwa kukiuka amri ya mahakama.

Shauri hilo limetajwa tena jana mbele ya Juma Hassan, Kaimu Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambapo alitoa hati nyingine kumuelekeza Kamanda wa Polisi Kanda ya Kinondoni kuwakamata wadaiwa hao.

Msajili Juma alitoa hati hiyo baada ya Mwesigwa Muhingo, Wakili wa Shekhe Mbonde,  kuomba hati hiyo ipelekwe Kinondoni kwa kuwa Babu Tale anaishi huko na si Wilaya ya Ilala kama hati ya kwanza ilivyoeleza.

Tarehe 18 Februari mwaka huu, Jaji Augustine Shangwa, aliwaamuru wadaiwa kulipa Sh. 200 milioni  kama fidia ya kuvunja haki miliki ya Shekhe Mbonde na Sh. 50 milioni kama fidia ya hasara aliyoipata kutokana na kuvunja makubaliano.

Katika uamuzi wake Jaji Shangwa alisema, Juni 16, 2013, Mbonde aliingia makubaliano na wadaiwa hao na wenzake ya kufanya biashara ya kurekodi mawaidha na kutengeneza nakala DVDs kwa ajili ya kuziuza nchini.

Wadaiwa hao waliahidi kumjengea nyumba, kumnunulia gari na kuitangaza kazi yake pia walimpa Sh milioni mbili na kumnunulia kanzu na kofia (baraghashia) na kurekodi DVDs zenye ujumbe Uzito wa Kifo, Fitina Juu ya Wanawake, Umuhimu wa Swala, Mwanadamu Yumo Ndani ya Hasara na Maadui wa Uislam.

Alisema, makubaliano ya awali yalikuwa kurekodi halafu baadaye wakubaliane kuhusu bei na jinsi ya kuziuza, badala yake waliziuza na kuzisambaza nakala hizo na kujipatia faida bila kumshirikisha Mbonde ambaye alitumia ujuzi wake.

Mbonde kupitia wakili wake Muhingo, Gwamaka Mwaikugile na Clement Kihoko,  alifungua kesi ya madai namba 185/2013 akiiomba mahakama iamuru wadaiwa wamlipe Sh. 700 milioni kama  fidia ya kuvunja makubaliano na Sh. 50 milioni kama fidia ya hasara aliyoipata kutokana na kuvunjwa kwa makubaliano.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuzindua upanuzi Uwanja wa Ndege Dodoma


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa leo atazindua awamu ya kwanza ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma ili uweze kupokea ndege kubwa za mizigo, abiria na viongozi wa kitaifa na kimataifa.

Uzinduzi huo ni miongoni mwa maandalizi ya kutimiza azma ya kuufanya mkoa wa Dodoma kuwa Makao Makuu ya Tanzania. Ujenzi huo unatarajia kugharimu Sh bilioni 11.5 ambazo ni fedha za ndani na utatoa fursa kwa mashirika ya ndege kuanza huduma Dodoma, ikiwemo ndege ambazo zitanunuliwa na serikali.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema, leo Waziri Mkuu atazindua awamu ya kwanza ya ukarabati wa uwanja huo kwa niaba ya Rais John Magufuli, na kuongeza kuwa uzinduzi huo hautaathiri mchakato wa kujenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa eneo la Msalato.

“Mchakato wa ujenzi wa uwanja wa ndege Msalato uko pale pale,”alisema Rugimbana na kuongeza kuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeamua kufanya upanuzi wa uwanja huo ili ndege kubwa zitue mkoani humo.

‘’Wizara ya Ujenzi imeamua kufanya upanuzi wa uwanja wetu wa ndege wa Dodoma ili ndege kubwa ziweze kutua na sisi tunamshukuru Rais kwa kutupa uwanja huo kwani utazidi kufungua fursa katika mkoa wetu,”alieleza Rugimbana.

Rugimbana alisema sababu ya kupanuliwa uwanja huo ni nia ya dhati ya Rais Magufuli ya serikali yake kuhamia Dodoma.

Alisema baada ya uzinduzi huo wa awamu ya kwanza, awamu ya pili itafanyika kwa haraka ili uwanja huo uweze kukamilika kama ilivyopangwa.

Upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma unahusisha njia ya kuruka na kutua kwa ndege, yenye urefu wa kilometa 2.5 na mita 500 za taa za kuongozea ndege na usalama wa kuruka kwa ndege.

Rais Magufuli amteua Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Sylvester Michael Mpanduji kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO).
 
Taarifa iliyotolewa jana Ikulu Jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Prof. Sylvester Michael Mpanduji umeanzia jana tarehe 18 Julai, 2016.
 
Kabla ya uteuzi huu Prof. Sylvester Michael Mpanduji alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
 
Prof. Sylvester Michael Mpanduji anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhandisi Omary Jumanne Bakari ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
 
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Dkt.Winnie Mpanju-Shumbusho kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa - Dodoma.
 
Kabla ya Uteuzi huo, Dkt. Winnie Mpanju-Shumbusho alikuwa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) lenye makao yake makuu Mjini Geneva nchini Uswisi na alimaliza mkataba wake tangu Mwezi Desemba 2015.
 
Uteuzi wa Dkt. Winnie Mpanju-Shumbusho umeanza jana tarehe 18 Julai, 2016.
 
Dkt. Winnie Mpanju-Shumbusho anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Donan William Mmbando ambaye ameomba kupumzika kutokana na sababu binafsi.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
18 Julai, 2016

Wakurugenzi 6 wa NSSF Wasimamishwa Kazi Kupisha Uchunguzi


BODI ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) imeagiza kusimamishwa kwa wakurugenzi sita, mameneja watano na mhandisi mmoja wa shirika hilo kupisha uchunguzi, kubaini wahusika katika tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na ajira.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Profesa Samwel Wangwe, alikiri  jana usiku kusimamishwa kwa vigogo hao 11, kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizoelekezwa kwao.

“Ni taarifa sahihi hizo. Kulikuwa na tuhuma katika ripoti ya ukaguzi, kwa hiyo tumeamua wakae pembeni ili kupisha uchunguzi, hawajafukuzwa kazi. Taarifa hiyo ya kusimamishwa ni sawa sawa,” alisema Profesa Wangwe jana usiku.

Kwa mujibu wa taarifa kwa wafanyakazi, iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, iliwataja wakurugenzi sita waliosimamishwa kuwa ni Yacob Kidula (Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi), Ludovick Mrosso (Mkurugenzi wa Fedha) na Chiku Matessa (Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala).

Wengine ni Sadi Shemilwa (Mkurugenzi wa Udhibiti Hadhara na Majanga), Pauline Mtunda (Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani) na Crescentius Magori (Mkurugenzi wa Uendeshaji).

Aidha, taarifa hiyo iliwataja mameneja waliosimamishwa kuwa ni Amina Abdallah (Meneja Utawala), Abdallah Mseli (Meneja wa Uwekezaji), Mhandisi John Msemo (Meneja wa Miradi), Davis Kalanje (Mhasibu Mkuu), Wakili Chedrik Komba (Meneja Kiongozi – Mkoa wa Temeke) na Mhandisi John Ndazi (Meneja Mradi).

Taarifa hiyo kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, ilisema kwamba uamuzi huo umefanywa na Bodi chini ya Profesa Wangwe iliyokutana Julai 15, mwaka huu kutokana na taarifa mbalimbali za wakaguzi wa hesabu na shughuli za uendeshaji wa shirika hilo la umma.

“Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii chini ya Uenyekiti wa Profesa Samwel Wangwe katika kikao chake cha 106 kilichofanyika tarehe 15 Julai, 2016 kimeagiza kusimamishwa kazi kwa wakurugenzi sita (6), mameneja watano (5) na mhandisi mmoja ili kupisha uchunguzi kubaini wahusika katika tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi na manunuzi ya umma na ajira,” ilieleza taarifa hiyo.

Hivi karibuni, NSSF ilitajwa katika vyombo vya habari kuhusu tuhuma zikiwamo za ununuzi wa ardhi usiofuata taratibu za manunuzi ya umma, kuwapo kwa ubadhirifu na ajira za upendeleo katika shirika hilo, ukiwataja wahusika kuwa ni baadhi ya wakurugenzi wa shirika hilo.



Older Posts
© Copyright MFUKUNYUZI | Designed By Code Nirvana
Back To Top